
Hell’s Kitchen ni eneo lenye umaarufu mkubwa katika Marafa, Malindi nchini Kenya. Eneo hili linajulikana kwa mandhari yake nzuri na kipekee. Hell’s Kitchen linajumuisha mabonde yaliyochongeka na kuwa miamba na maumbo ya ajabu, ambayo hutoa picha ya kuvutia.
Vitu vya kuzingatia:
Tafadhali tembelea Hell’s Kitchen wakati wa asubuhi na baada ya saa 2:30 alasiri. Unauliza kwa nini? Jina linatoa sababu. Wakati wa mchana, mahali hapa huwa na joto jingi sana hadi nyuzi 50⁰. Kwa hiyo, inashauriwa sana kutembelea baadaye alasiri wakati joto limepungua ili uweze kufurahia kikamilifu.
Kumbuka kuwa na chupa ya maji kwani utaihitaji sana.
Kihistoria, Hell’s Kitchen imekuwa kituo cha kuvutia kwa wageni na watalii kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu. Inasemekana kuwa eneo hili lilikuwa linatumika kama shamba la mapigano ya wakoloni wa Kijerumani na Waingereza wakati wa zamani. Jina “Hell’s Kitchen” linasemekana limepewa eneo hili kutokana na hali yake ya joto kali na ukame, ambayo ilifanya kuwa vigumu kuishi hapo.
Kama unavyojua, kila sehemu ina historia ya kutokea au kuwa kwa hali hiyo. Hell’s Kitchen ina historia yake. Inasemekana kuwa hapo zamani kulikuwa na familia ya Kizungu katika kijiji cha Marafa. Ilikuwa siku moja, maji yakakosekana. Familia hii ilikuwa tajiri na wenye mifugo wengi. Hivyo, kutokana na ukosefu huo wa maji, waliamua kutumia maziwa kama mbadala wa maji. Walitumia maziwa katika shughuli zote kama vile kuoga, kufua, na kadhalika. Hali hii iliwakera wakaazi na hata Mungu. Mungu akaporomosha sehemu hiyo pamoja na familia hiyo.
Historia ya sehemu hii inadhibitishwa kutokana na uwepo wa rangi tatu tofauti ya mchanga. Kuna rangi ya manjano, nyeupe, na nyekundu. Inasemekana kuwa rangi nyekundu inawakilisha damu iliyomwagika na nyeupe inawakilisha maziwa.
Mandhari ya Hell’s Kitchen ni ya kuvutia sana. Unapoingia eneo hilo, utakutana na mabonde yenye rangi tofauti ya ardhi, kutoka kahawia hadi nyekundu, na maumbo ya ajabu ya miamba iliyochongwa na mmomonyoko wa asili. Mambo ya miamba katika Hell’s Kitchen inabadilika kila uchao kutokana na mmomonyoko wa udongo wakati wa mvua. Hali inawezesha mwonekano wa kupendeza na mambo ya ajabu.
Eneo la Hell’s Kitchen limekuwa maarufu sana kwa wapenzi wa asili na watalii wanaotafuta uzoefu wa kipekee. Wageni wanaweza kufurahia kutembea kando ya mabonde, kuchunguza maumbo ya miamba, na kufurahia mandhari ya kushangaza. Pia, ni mahali pazuri kwa wapiga picha kupata picha nzuri za asili.
Kwa ujumla, Hell’s Kitchen ni eneo lenye historia ya kuvutia na mandhari ya kipekee nchini Kenya. Ni mahali pazuri kwa watalii kutembelea na kujionea uzuri wake wa kipekee.





Natumai kweli nimeelezea kwa ufasaha hazina hii nzuri iliyofichika na kwamba umeona thamani katika makala hii na una hamu ya kuitembelea.

Leave a comment