AINA ZA MANENO

Aina za maneno
Kuna mijadala kadhaa kuhusu idadi halisi ya aina za maneno katika lugha, wapo wanaoamini kuwa aina za maneno zipo saba na wengine wanadai zipo nane. Katika andiko hili sitajihusisha kabisa na mjadala huo isipokuwa nitafafanua idadi nane za aina za maneno zinazoelezwa na wengi. Hivyo zifuatazo ni aina nane za maneno katika lugha ya Kiswahili.
Nomino (N)
Vitenzi (T)
Viwakilishi (W)
Vivumishi (V)
Vielezi (E)
Viunganishi (U)
Vihusishi (H) au Vibainishi
Vihisishi (I)

NOMINO
Nomino ni maneno yanayoeleza majina ya watu, vitu, mahali, hali, tabia au taratibu. Kwa mfano, Fatma, uvivu, nyumbani. kuna aina sita za Nomino ambazo nitazifafanua hapa chini.

AINA ZA NOMINO
1.Nomino za Kipekee
Nomino ambazo hutaja vitu vya kipekee. Nomino hizi hutaja kitu kwa kukitambulisha waziwazi kwa jina au majina yake kamili. . Majina haya huanza Kwa herufi kubwa ima iwe mwanzoni mwa sentensi au hata katikati. Nomino hizi hazina wingi.

  • Mfano Kenya, Otieno nk.
  1. Nomino za Jumla (Nomino za Kawaida)
    Hizi ni nomino zinazotaja kitu bila kukitambulisha kwa jina lake halisi. Kwa mfano kama ni mji hatuambiwi ni Nairobi au Mombasa. Nomino hizi huanza kwa herufi ndogo isipokuwa tu zinapotokea mwanzoni mwa sentensi.
  • Mfano wa nomino za kawaida, nchi, kitabu, Chakula,mtu, nk.
  1. Nomino za Jamii au makundi
    Nomino za vitu vinavyotokea kwa makundi. Kila kundi hurejelewa kwa kutumia jina au nomino maalum.
  • Kwa mfano, umati wa watu, thurea,genge,Baraza,msafara,tita la kuni nk.
  1. Nomino za wingi
    Nomino hizi hutokea tu kwa wingi. Haziwezi kugawika ili ziwe kitu kimoja kimoja.
  • Kwa mfano, mazingira, mali, madini, kelele, maziwa, maji nk.
  1. Nomino dhahania
    Majina ya vitu vya kufirika tu wala haviwezi kugusika, kuonjeka au kuonekana.Havina umbo halisi.
  • Kwa mfano, Malaika, Shetani, furaha, huzuni, wasiwasi nk.
  1. Nomino za Vitenzi jina
    Nomino zinazoundwa kutokana na vitenzi. Huundwa kwa kuongezewa kiambishi ‘ku_’ mwanzoni mwa mzizi wa kitenzi.
  • Kwa mfano, kupika, kucheza, kuchora, kuimba n.k
    Kucheza kwake kunafurahisha.
    VITENZI
    Vitenzi ni maneno yanayoarifu kuhusu jambo linalotendwa au kutendewa nomino. Vitenzi huwa na mzizi ambao kwamba ndio unaosimamia tendo lenyewe na mzizi huo huambatanishwa na viambishi ili kuleta maana inayokusudiwa. Kwa mfano, alipita.
    A-li-viambishi awali
    pit-mzizi
    a- kiambishi tamati

AINA ZA VITENZI
1.Vitenzi halisi (T)
Vitenzi halisi ni vitenzi ambavyo hutarifu au kufahamisha kuhusu jambo linalotendawa. Sifa muhimu kuvihisu ni kwamba vitenzi hivi huwa na viambishi kabla na baada ya mzizi wa kitenzi.Viamboshi hivi huwakilisha nafsi, wakati, mtendaji au kiishio.
Vitenzi hivi huonyesha kitendo halisi, kikubwa au muhimu kilichotendwa na mtendaji. Kwa mfano, mama anapika pilau.
Mifano zaidi:
Sisi tutalima shamba letu.
Mimi ninakula chakula kitamu.
Paka amemkamata panya.
Mwanafunzi alisoma kitabu cha hadithi.
Wewe utaimba wimbo mzuri.
Mkulima anavuna mahindi.
Kiti kitabebwa na mtoto.
Nyumba ilijengwa mjini.
Suruali imefuliwa.

  1. Vitenzi visaidizi (Ts) na Vitenzi Vikuu.
    Vitenzi visaidizi na Vikuu hutumika pamoja. Husaidiana na vitenzi vikuu ili kitendo kilichotendwa kifafanuliwe au kieleweke zaidi. Vitenzi visaidizi hubeba kiambishi Cha nafasi na wakati ambapo Vikuu hubeba wazo kuu linalowasilishwa.
    Kwa mfano;
    Mwalimu alikuwa(Ts) anafunza(T. Kikuu) hisabati.
    Wazee walikuwa(Ts) Wakilima(T. Kikuu) siku hiyo.
    Polisi waliweza(Ts) kujua(T. Kikuu) ukweli.
  2. Vitenzi vishirikishi
    Vitenzi vinavyoshirikisha vitu kihali, kitabia au kimazingira. Kwa mfano:
    Vedasto ni mvulana mtiifu.
    Mwalimu wetu si mkali.
    Yule ndiye mwanafunzi aliyeibuka wa kwanza.
    Sisi tu mabinti wenye msimamo.

Vitenzi vishirikishi vimegawanyika katika aina mbili:

a) Vitenzi vishirikishi vikamilfu: Hivi vinaweza kuchukua viwakilishi nafsi au viambishi vya ngeli na pia viambishi vya wakati. Ni maneno kama, weza, kuwa, kwisha, kuja, taka, ngali, pasa, bidi, pata na kwenda. Kwa mfano:
Mtoto amekuwa kwa shangazi yake.
Kijana yule anapaswa kuwa hospitalini.

Vitenzi vishirikishi vikamilifu mara nyingine huweza kutokea kama vitenzi visaidizi iwapo vinatokea sambamba na vitenzi vikuu. Kwa mfano:
Mpishi alikuwa anapika.
b) Vitenzi vishirikishi vipungufu: vitenzi hivi haviwezi kuchukua viambishi vya wakati ingawa vinaweza kuchukua viwakilishi nafsi viambata au viambishi nngeli.kwa mfano:
Sharifa ni msichana mrembo.
Yule si mtoto mtukutu.
Gari li maegeshoni.

  1. Vitenzi Sambamba.
    Ni Vitenzi vya hadhi Moja au sawa vikitumika pamoja na kuwa ubavu Kwa ubavu katika sentensi. Kwa mifano:
    Mimi sikumruhusu akirarue ki’tabu hicho.
    Tulitahiniwa, tukarudishiwa madaftari na tukapongezwa.

VIWAKILISHI
Viwakilishi ni maneno yanayotumika badala ya nomino(vibadala vya nomino). Nomino husika huwa haitajwi katika sentensi. Kwa mfano,
Yule ni mtunzi mbuji wa mashairi.

AINA ZA VIWAKILISHI

  1. Viwakilishi vya nafsi
    Hivi ni viwakilishi vinavyosimamia viumbe vyenye uhai na hutokea ima katika nafsi ya kwanza, nafsi ya pili au nafsi ya tatu.
  • Kwa mfano:
    Mimi ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Masinde Muliro
    Wewe ni mama bora.
    Yeye ni ghulamu mtanashati.
    Kuna aina mbili kuu ya viwakilishi vya nafsi:

a) Viwakilishi nafsi huru: Hivi ni viwakilishi visivyohitaji kuongezewa viambishi vyovyote ili kujikamilisha. Navyo ni; mimi, sisi, wewe, nyinyi, yeye, wao.

b) Viwakilishi nafsi viambata (vitegemezi): Hivi ni viwakilishi vinavyotokea kama viambishi. Si maneno huru. Kwa mfano;
Nilikula chapati tamu sana .
Anatarajiwa kufika leo.

  1. Viwakilishi vya ngeli
    Hivi ni viwakilishi vinavyoonyesha kuwa nomino inayohusika imo katika ngeli fulani. Kwa mfano:
    Kilichopikwa ni chetu sote.
    Yatafungwa jioni.
    3.Viwakilishi vya sifa
    Haya ni maneno ya sifa yanayosimamia nomino. Kwa mfano,
    Wakubwa wasubiri wadogo wale
    Mzuri amezaliwa leo.
    Safi imeandikwa nje.
    Mifano zaidi; safi, Dunia, hafifu, ghali, stadi, – zuri, -baya, -pya, -ema n.k

4.Viwakilishi vya A-Unganifu
Viwakilishi hivi hushirikisha majina mawili yenye uhusiano na hujengwa kwa kutumia A-unganifu. Kwa mfano, Wa zizini atachinjwa kesho.
Mifano: la, wa, Cha, mwa, vya, Kwa, pa, ya n.k

  1. Viwakilishi vya pekee
    Haya ni maneno yalioundwa kutokana na mzizi ‘-ingine’, ‘-ote’, ‘-o-ote’, ‘-enyewe’ na ‘-enye’ ‘- ingine-o’ na kutumika kama viwakilishi. Kwa mfano:
    Lolote linakubalika.
    Wenyewe waliingia nyumbani.
    Mwenye kipaji cha kutunga mashairi amezawadiwa.
  2. Viwakilishi virejeshi
    Viwakilishi vinavyoundwa kutokana na kiambishi ‘o-rejeshi‘ au amba-.
    Hurejelea kinachowakilishwa. Kwa mfano:
    Wanaokula ni wanangu
    Nguo ambayo ulinipa ilinitosha sawa sawa.
  3. Viwakilishi visisitizi
    Hivi ni viwakilishi vinavyotumika kusisitiza nomino ambayo yenyewe haitajwi katika sentensi. Kwa mfano, Mwalimu anatumia Kiki hiki.
    Mifano zaidi:
    Yuyu huyu.
    Uu huu.
    Yaya haya.
    Lili hili.
    Papa hapa. n.k kutegemea ngeli husika.
    8.Viwakilishi vimilikishi
    Hivi ni viwakilishi vinavyoonyesha umilikaji. Msingi wake ni mizizi ya vimilikishi nafasi.
    Kwa mfano, Chake kimepotea.
    -angu
    -ako
    -ake
    -etu n.k
  4. Viwakilishi viulizi
    Viwakilishi hivi hutumika katika swali. Kusudi ni kubainisha mtendaji au mtendwa. Mashina yake ni -ipi na -ngapi.
    Kwa mfano,
    Nani ameenda sokoni?
    Upi umekatwa?
    Lipi limechanua?
  5. Viwakilishi vya idadi
    Hivi ni viwakilishi vinavyoonyesha idadi halisi au jumla yakichukua nafasi ya nomino.
    Kwa mfano,
    Vinne vinatosha.
    Wengi walihudhuria mahojiano.
    Chache zitarekebishwa kesho.

11.Viwakilishi vionyeshi
Hivi ni viwakilishi vinavyoashiria kitu kinachozungumziwa.
Kwa mfano,
Yule alinisaidia sana.
Kile kitarekebishwa.
Huo umejengwa.
Huu umefungwa.

VIVUMISHI
Kivumishi ni neno au fungu la maneno linaloeleza zaidi juu ya nomino. Kivumishi ‘huvumisha’, yaani hueleza mtu namna alivyo au kitu nama kilivyo, kinavyofikirika au kufikiriwa. Pia huonyesha idadi fulani ya kile kinachozungumziwa. Kuvumisha ni kutoa habari.

Tunaweza pia tukasema, vivumishi ni maneno yanayosifu au kufasili sura za nomino.

AINA ZA VIVUMISHI

  1. Vivumishi vya sifa
    Haya ni maneno yanayotaja sifa au tabia ya nomino inayovumishwa. Kwa mfano, Mtoto mzuri amefaulu mtihani.
  2. Vivumishi vya idadi
    Hivi ni vivumishi vinavyoonyesha idadi ya nomino zinazozungumziwa. Vivumishi hivi huweza kuwa:
    Vya idadi mahsusi/maalum (idadi dhahiri). Kwa mfano, wanafunzi wawili walishiriki mashindano ya uandishi wa insha.
    Vya idadi ya jumla(idadi isiyodhahiri). Kwa mfano, watu wengi walihudhuria harusi hiyo.

3.Vivumishi vioneshi (Vya ishara)
Vivumishi vinavyotumika kuonyesha mahali kitu kilipo kwa njia ya kuashiria. Kwa mfano, Gari lile liliegeshwa karibu na duka kuu.

  1. Vivumishi viulizi
    Vivumishi vinavyodhihirisha kuwepo kwa swali. Hutumiwa ili kuuliza swali kuhusu nomino. Kwa mfano, Rahma amejifungua mtoto gani?
  2. Vivumishi vimilikishi
    Vivumishi hivi huelezea ni nani anayemiliki nomino. Kwa mfano, Kikombe changu ni kidogo.
  3. Vivumishi vya majina
    Hizi ni nomino ambazo hutumika kama vivumishi. Hutumika ili kuelezea zaidi maana ya majina mengine. Vivumishi hivi vikiwa peke yake huwa ni majina tu, lakini vikiunganishwa na majina mengine hufanya kazi ya wasifu (yaani kusifu) au kuelezea jina linalotangulia.
    Kwa mfano,
    Mwanamke tajiri amekuja shuleni.

Tajiri ni nomino iwapo itatumika bila neno mwanamke. Kwa mfano, tajiri amekuja shuleni.

  1. Vivumishi vya pekee
    Hivi hutokana na mizizi ‘-ote, -o-ote, -ingine, -enye na -enyewe’. Kwa mfano, Wanafunzi wengine wamefika shuleni.
  2. Vivumishi vya A-Unganifu
    Hivi ni vivumishi vinavyoundwa kwa a-unganifu na hutumika kutoa sifa za nomino. Kwa mfano, daftari la mwalimu lipo juu ya meza.
  3. Vivumishi virejeshi
    Hivi ni vivumishi vinavyotumika kurejelea nomino. Hujengwa kwa kutumia ‘O-rejeshi’. Kwa mfano, mtoto huyo alikunywa uji wa wimbi.
  4. Vivumishi vya kusisitiza/ sisitizi
    Hivi hutumika kusisitiza nomino iliyotajwa hapo awali. Kwa mfano, Daftari lili hili ndilo alilotumia.

VIUNGANISHI
Viunganishi ni maneno yanayotumiwa kuunganisha vipashio mbali mbali vya lugha. Kwa kawaida, huunganisha vipashio vifuatavyo:
Neno na neno
Kirai na kirai
Kishazi na kishazi
Sentensi na sentensi
AINA ZA VIUNGANISHI

  1. Viunganishi vya sababu
    Viunganishi hivi huunganisha hali moja na sababu yake.
    Kwa mfano,
    Aliadhibiwa kwa sababu alichelewa.
    Kwa maana, Kwa kuwa, kama, Kwa vile, kwamba, Kwa hivyo n.k
  2. Viunganishi vya masharti
    Viunganishi hivi huunganisha hali na masharti ya hali hiyo.
    Kwa mfano, iwapo atamaliza mitihani mapema, ataenda kwa shangazi yake.
    Kama, n.k
  3. Viunganishi vya tofauti
    Viunganishi hivi huonyesha tofauti baina ya kitu/hali moja na nyingine.
    Kwa mfano, wanafunzi wote wamefaulu mtihani isipokuwa wanafunzi wawili.
    bali, ingawa, pamoja,lakini, ila,Wala, ilhali n.k
  4. Viunganishi vya kuteua/Kuchagua
    Hivi hudhihirisha uchaguzi au uteuzi baina ya vitu viwili au zaidi.
    Kwa mfano, utaenda Malindi au Lamu?
    Ama, Wala n.k
  5. Viunganishi vya ziada
    Hivi huonyesha hali au vitu vya ziada, licha ya vile vilivyotajwa mwanzo.
    Kwa mfano, na, pia, aidha, licha, pamoja na.

Mifano katika sentensi:
Alikula chapati, viazi vya nazi na sambusa.
Licha ya kuwa mwanauchumi, ni mwandishi.

  1. Viunganishi vilinganishi
    Hivi hulinganisha vitu viwili au zaidi. Kwa mfano: Sembuse, kuliko, zaidi ya, seuze.

Mifano katika sentensi:
Anapenda chapati kuliko wali.
Umeshindwa kuamka saa moja asubuhi, seuzi saa kumi alfajiri?

  1. Viunganishi vya kujumlisha.
    Huonyesha dhana ya kujumlisha. Kwa mifano:
    Wewe na Mimi tunasikizana.
    Pia, tena, juu ya hayo, fauka ya, pamoja na n.k

Vielezi (E)
Kielezi ni neno linaloeleza zaidi kuhusu kufanyika kwa tendo. Viele hujibu maswali kama: (a) tendo lilifanywa namna gani? (b) tendo lilifanywa lini au wakati gani? (c) tendo lilifanywa kwa njia gani? (d) za vielezi. Vielezi hidan hinhwa wapi? (e) tendo lilifanynbalimbali gapi?n.k. Maj ya maswali haya ndiyo msingi wa aina mbalimbali Navibusu vitenzi tu bali huweza kuhusu vivumishi na vingine

(a) Vielezi vya namna au jinsi
Hivi ni vielezi ambavyo hueleza jinsi au namna jambo linavyofanywa yaani hujibu swali- lilifanyika namna gani? Kwa mfano:

  1. Masabu alikasirika sana.
  2. Keah alicheza kayamba vizuri.
  3. Barre alisema vibaya.
    Kuna aina mbalimbali za vielezi vya jinsi au namna kutokana na sifa zake tofauti. Aina hizo ni:
    (1) Vielezi namna hali
    (ii) Vielezi vya namna mfanano
    (iii) Vielezi vya namna halisi
    iv) Vielezi vya namna vikariri
    (v) Vielezi vya namna ala
    (vi) Vielezi vya namna viigizi
    (vii) Vielezi vya mahali

(i) Vielezi vya namna hali
Hivi ni vielezi ambavyo hueleza tendo lilitendeka kwa namna au jinsi gani. Mifano:
(1) Juma alifyatuka mbio.
(2) Mzee wa Madafu alilewa chakari.
(3) Wanafunzi waliimba vizuri.

(ii) Vielezi vya namna mfanano
Vielezi hivi huelezea jinsi ya kutendeka kwa tendo kwa kufananisha na vivumishi au nomino mbalimbali. Ili kuleta ufananisho huu, huwepo matumizi ya ki-. Mifano:
(1). Alimtendea kinyama.
(2). Otieno alicheza kishujaa.
(3). Yule kiongozi alitawala kihayawani.

(iii) Vielezi vya namna halisi
Hutumiwa kuelezea vielezi vitokanavyo na maneno ambayo kiasili au kikawaida ni vielezi. Katika lugha kuna maneno ambayo kiasili ni vielezi na mengine ambayo ingawa si vielezi huweza kutumiwa kama vielezi. Mifano:
(1.) Kimani aliifanya kazi ile barabara.
(2.) Madzayo aliongea ovyo.
(3.) Ujanja wake ulimwishia kabisa.

(iv) Vielezi vya namna vikariri
Vielezi hivi huelezea vitenzi kwa kurudiarudia, yaani vinakariri kwa kuwapo marudio ya neno moja. Mifano:
(1.) Dumu la Maimuna lilianguka na kuvunjika nyaka nyaka.
(2.) Nilipomdai pesa zangu alinijibu kimzahamzaha.
(3.) Usipende kusoma hivi hivi bila ya mpango.

(v) Vielezi namna ala
Hivi ni vielezi ambavyo hutaja kitu ambacho kinatumika au kilitumika kufanyia tendo fulani. Mifano:
(1) Mnyama alipopigwa mshale na mwindaji alianguka.
(2) Kimau alidungwa mwiba na mwenzake.
(3) Wangotta alimpiga bakora kijana aliyemchezea dadake.

(vi) Vielezi namna viigizi
Hivi ni vielezi ambavyo hueleza tendo kwa kuiga ule utendekaji wake. Mifano:
(1) Wanjiru aliukomea mlango kome.
(2) Nyagah alianguka majini chubwi.
(3) Katama alitega masikio ndi kuisikiliza taarifa ya habari..

(vi) Vielezi vya mahali
Hueleza tendo lilifanywa wapi. Mifano:
(1) Mama amekwenda sokoni.
(2) Kesho tutasaafiri Mombasa.

Vielezi vya wakati
Vielezi vya wakati hueleza tendo lilitendeka au kufanyika wakati gani. Je, lilitendeka siku, mwezi, mwaka au majira gani. Vielezi hivi hutokana na matumizi ya maneno kamili au kwa kuwepo kwa viambishi vinavyohusishwa na wakati.

(i) Vielezi vya wakati vya maneno kamili
(a) Michira aliondoka jana.
(b) Farida alirudi usiku.
(c) Moraa alisema angemjibu kesho.
(d) Nitarudi punde.

(ii) Vielezi vya viambishi
Vielezi hivi huonyeshwa na kuwepo kwa {po}
(a) Tulipata chajio mama alipowasili.
(b) Alipofika nyumbani, hakumkuta yeyote.
(c) Mtoto aliapo, mama humpa maziwa.
(d) Juma achezapo mpira, watu humshangilia.
Vielezi vya idadi/ kiasi
Vielezi vya idadi au kiasi hueleza ni mara ngapi tendo linalozungumziwa lilitendeka. Hueleza pia kiasi kinachohusika. Idadi hiyo inayoweza kuwa halisi au wazi au ikawa ya kijumla. Tuangalie mifano hii:
(1) Vielezi vya idadi halisi
(a) Mutua alimpiga Kilo mara tatu.
(b) Anahitaji wiki kuifanya kazi ile.

(ii) Vielezi vya idadi ya jumla
(a) Gichovi analalamika daima.
b) Debe lilijaa pomoni.
(c) Mwasimba alilimega lile gogo kidogo.

Vielezi vya mahali
Vielezi vya mahali hutumiwa kuonyesha tendo linafanyika wapi. Vielezi hivi huonyeshwa kwa matumizi ya maneno kamili au kwa viambishi vya mahali {po} {ko} na {mo} pamoja na kiambishi tamati {-ni). Tuangalie mifano ifuatayo:
(i) Vielezi vya mahali vya maneno kamili (a) Wale wafanyakazi wanaishi hapa.
(b) Simba aliyemshambulia mtoto anajificha pale.
(c) Vitabu huhifadhiwa juu.
(d) Manamba alilibwaga gunia chini.

(ii) Vielezi vya mahali vya viambishi
(a) Tulikwenda nyumbani.
(b) Sijui alikokwenda Juma.
(c) Ndugu yake alikofikia ni hoteli ya Sirikwa mjini Eldoret.
(d) Alipokuwa palikuwa na ajali.
(e) Humo mna hatari.
(f) Wanacheza uwanjani.

Tanbihi: Maneno yote ya mlazo (katika mifano hapa juu) ni vielezi. Ni viambishi ni, ko, po na mo ndivyo hasa vinavyoonyesha dhana ya mahali katika maneno hayo.
Vihisishi (I)

Maneno haya hutumiwa kuonyesha hisia kama vile:

(i) Mshangao-Salaale! Loo! Ahaa! Aka! Kumbe! Ala! Lahaula!
(ii) Huruma-Maskini!
(iii) Majuto – Ole wangu!
(iv) Makubaliano au hamu ya kutaka mtu aendelee kuzungumza -Ehee! Hewa! Ambal Ahaa!
(v) Kubeza/kudharau-Aka! Etil
(vi) Furaha – Alhamdulilahi! Loo! Haleluya!
(vii) Hasira – Kefle! Ah! He!
(viii) Kutahadharisha – Hel Aisee!
(ix) Kusisitiza – Hata!

Vihusishi.
Kihusishi ni neno au fungu la maneno ambalo huonyesha uhusiano baina ya kitu na kingine au mtu na mwingine. Uhusiano huu unaweza kuwa wa mahali, wakati, au kiwango.
Kuma aina mbalimbali za vihusishi kama vile:

  1. Vihusishi vya wakati
    Mifano
    tangu
    hadi
    baada ya
    mpaka
    kabla ya
    toka

Mifano katika sentensi:
(a) Kiongozi aliondoka baada ya kuhutubu.
(b) Wao hawajarudi hapa tangu wasafiri.
(e) Ataendele kuvujiwa mpaka siku ataiezeka nyumba hiyo.
(d) Tulishinda na kiu hadi ulipowasili.
(e) Hawajatuletea habari yoyote toka walipoondoka.

  1. Vihusishi vya mahali
    Hivi ni vihusishi vinavyoonyesha uhusiano wa mahali.
    Mfano
    katika
    juu ya
    kando ya
    chini ya
    ndani ya
    mvunguni mwa

Mifano katika sentensi
(a) Nilimkuta ameketi kando ya nyumba.
(b) Vito vya dhahabu vimo ndani ya kasha.
(c) Paka alilala mvunguni mwa kitanda.
(d) Bilauri iko juu ya meza.
(e) Pesa hizo zimepatikana katika nyumba yake.

  1. Vihusishi vya kiwango
    Hivi ni vihusishi ambavyo huhusisha vitu kwa kuvilinganisha labda kwa kutegemea zito, nguvu au kufaulu.
    Mifano:
    zaidi ya
    mithili ya
    sawasawa na
    kati ya

Mifano katika sentensi
(a) Amechuma matunda zaidi ya rafiki yake.
(b) Walikimbia mithili ya swara.
(c) Tutafanya kazi sawasawa na wenzetu.



2 responses to “AINA ZA MANENO”

  1. Mashinloo Salim Avatar
    Mashinloo Salim

    Mashaallah, kazi safi sana ndugu yangu Rop Nickolus, you are a 1st Class Honours, and you deserve it.

    Liked by 1 person

    1. Asante sana Guru wa Kiswahili na Mashairi.

      Like

Leave a comment

About Me

Welcome to my blog, MTU KUZI, a space dedicated to informing and educating a diverse audience without bias toward age, gender, race, or any other distinguishing factor. I am a seasoned professional with a deep foundation in communication, translation, administration, and education. My extensive experience spans prestigious roles at institutions like Pwani University, Mozilla Foundation, KIPPRA, and teaching Kiswahili at the University of Carolina – Chapel Hill.As a Kiswahili expert, I specialize in translating between English and Kiswahili and tutor both languages with a focus on immersive, practical learning experiences. My expertise in Kiswahili not only enhances my teaching but also enriches my translations, allowing for culturally and contextually accurate communication.In this blog, I leverage my skills and experiences to create content that bridges cultural divides and fosters understanding. Proficient in various software applications and online collaboration platforms, I aim to streamline communication processes and engage with a global audience effectively.You are invited to join me on this journey of exploration and learning. Follow MTU KUZI on Facebook, Twitter, Instagram, and LinkedIn to stay updated and connected. Thank you for visiting, and I look forward to sharing more with you.

Newsletter