

Paul McKenzie Nthenge ni Mchungaji wa Kanisa la ‘Good News International Church.
Alianza kanisa hili mwaka 2003 kama kituo kidogo cha kiinjilisti pamoja na mkewe Joyce Mwikamba.
Kisha walihamia kijiji kiitwacho Migingo huko Malindi ambako alianzisha kanisa katika boma lililozungukwa na ukuta, ambapo familia yake bado inaishi hadi sasa. Mkewe Joyce alisaidia katika kuhubiri kama mchungaji mwenza na McKenzie alidai kuwa na uwezo wa kuzungumza na Mungu MOJA KWA MOJA. Katika mahubiri yake, alidai kutoa maneno kama yalivyotolewa na Mungu mwenyewe.
Mnamo mwaka wa 2016, Mckenzie alipata kituo cha televisheni baada ya mmoja wa wafuasi wake Kennedy Mwacharo kuuza mali yake huko Lamu kwa bei ya kutupa ya Milioni 20 na kumkabidhi pesa zote huku akiacha familia na majukumu yake. Mali hiyo ilikuwa na thamani ya zaidi ya Milioni 100 wakati huo. Kinachoshangaza ni kuwa Mwanamume huyo alifariki miezi miwili baadaye katika hali isiyoeleweka.
Kumekuwa na Kesi kadhaa za watu kuuza mali zao na kumpa Mchungaji McKenzie wakati wakingojea kukutana na Yesu. Hivi karibuni kisa Cha Betty, mhudumu wa Ndege au ‘air hostess’ ambaye aliacha kazi yake ya miaka 11, mumewe na kuuza uwekezaji wake kwa bei ya kutupa. milioni 7, Kisha aliondoka na fedha hizo na kuenda kanisa la McKenzie la Shakaola.
Betty anashukiwa kuwa miongoni mwa maiti zinazofukuliwa kwenye makaburi tatanishi huko Shakahola.
Inadaiwa kuwa McKenzie alitumia pesa ambazo Kennedy Mwacharo alimpa kununua vipande vya ardhi huko Malindi na Mombasa, magari mawili na kuanzisha kituo cha runinga. Kupitia kituo chake cha runinga, Mckenzie aliwafikia watu wengi sana na mafundisho yake kimsingi yalikuwa juu ya nyakati za mwisho, kuiga njia potovu za maisha za kimagharibi kama vile huduma za matibabu, elimu, chakula, michezo, muziki n.k.
Mackenzie alishikilia kauli ya kutokuwa na maana ya maisha na alisisitiza juu ya maisha ya baadaye. Alihubiri kuhusu ujio wa pili wa Kristo ambao kulingana naye ulikuwa hivi karibuni. Pia alikazia fikra ghadhabu iliyowangojea wale ambao wangekuwa hai kufikia wakati huo.
Mnamo mwaka wa 2018 Dkt. Ezekiel Mutua kupitia KFCB aliamuru kufungwa mara moja kwa kituo hicho cha runinga, hii ilikuwa mwaka mmoja baada ya Mckenzie na mkewe kufikishwa mahakamani kwa itikadi kali za kidini.
Haijulikani jinsi kesi hii iliisha na licha ya maagizo ya kufungia kituo cha runinga McKenzie aliendelea nayo jambo lililoonyesha kwamba huenda mizizi yake ilikuwa imeenea sana na kuwa na uwezo mkubwa. Kumbuka wakati fulani, alimtishia aliyekuwa Mbunge wa Kilifi wakati huo Aisha Jumwa alipohoji baadhi ya mafundisho yake na kwa nini aliwaweka wagonjwa katika boma lake badala ya kuwapeleka hospitalini.
Mnamo 2019, McKenzie alichipuka na kugonga vichwa vya habari tena wakati ndugu wanne kutoka Mumias waliondoka nyumbani kwenda kanisani kwake na kutoweka, hata hivyo, watatu kati yao waliibuka tena baadaye. Pia kulitokea na shinikizo lililowekwa juu yake kufungwa Kwa shule ambayo haikuwa imesajiliwa aliyokuwa akiendesha katika boma lake. Hii ikawa msukumo kwake kuhama kutoka Migingo hadi Shakaola. Alifunga kanisa, akauza baadhi ya magari yake kisha akanunua shamba la Shakaola kwa jina la kuanzisha biashara ya kilimo.
Watu waliokwenda kumuona katika kanisa lake la awali lililokuwa Migingo walielekezwa kwenda shambani kwake Shakaola na kulingana na majirani, watu wengi walienda huko lakini wachache walirudi. McKenzie alikuwa na watu wake wa mikono waliosimamia na kufuatia Hali ya wale walioshurutishwa kufungwa na kukaa bila chakula hadi walipofariki. Hawa pia ni watu wale wale wanaofanya kazi ya kuzika kwa ajili yake.
Inadaiwa kuwa wakati akitoka Migingo na kufunga kanisa lake, aliuza kituo cha Runinga (vifaa) na gari lake moja kwa Mchungaji Ezekiel wa Kanisa maarufu ya ‘New Life’ na hata baadhi ya vifaa vyake vya uinjilisti.
Kumbuka kuwa Mchungaji McKenzie haishi na familia yake huko Shakaola, familia hiyo inaishi katika kijiji cha Migingo katika eneo aliyokuwa amejenga kanisa lake awali.
Inasikitisha kuwa wakati huu wote akitenda unyama familia yake inaishi Maisha bora zaidi huku Wafuasi wakifa wanapojitayarisha kwa Safari ‘takatifu’. Kumbuka wengi wa watu hawa wanafunga msituni mchana na usiku, wakikabiliwa na hali mbaya ya hewa na hatari nyinginezo.

Leave a comment