WIKI YA LUGHA ZA KIAFRIKA: Kiswahili Kinavyokuza Uchumi Na Kuunda Nafasi Za Kazi Afrika
NA FAUSTINE NGILA
UMEWAHI kutambua tabia ya baadhi ya Wakenya kuwa ukisema nao kwa Kiswahili sanifu watakujibu tu kwa Kiingereza?
Nia yangu si kudhalilisha wanaotumia Kimombo kwa mazungumzo yao, ila kukuonyesha jinsi kukijua Kiswahili mufti kunavyoweza kukukweza katika daraja ya kiuchumi.
Hivi sasa Kiswahili kinafundishwa nchini Afrika Kusini. Hii inamaanisha iwapo wewe ni Mkenya aliye na ujuzi wa kipekee wa lugha hii, basi ukitua Johannesburg una fursa ya kujichumia hela kwa kufundisha Kiswahili katika shule za nchi hiyo.
Katika miaka michache ijayo, Afrika Kusini itahitaji maelfu ya walimu wa Kiswahili. Kikiwa lugha rasmi ya mataifa yote 54 ya Muungano wa Afrika (AU), Kiswahili kinatarajiwa kuzalisha mamilioni ya nafasi za ajira kwa walimu wanaoienzi lugha hiyo.
Na si mafunzo ya darasani pekee. Kuna majukwaa ainati ya mitandaoni ambayo tayari yanatumika kufundisha Kiswahili. Hii inamaanisha iwapo unaishi Nairobi, unahitaji tu intaneti na kipakatalishi kuwafunza wanafunzi 200 jijini Lagos, Nigeria.
Kwa walimu wa Kiswahili au wanafunzi wanaosomea Kiswahili katika vyuo vikuu, mamilioni ya hela yanawasubiri kutokana na huduma hii. Ajira zinazotokana na umilisi wa Kiswahili si mafunzo tu, pia kuna kazi zinazolipwa fedha nyingi kama vile ukalimani na utafsiri.
Mashirika ya habari kwa sasa yamemwaga mabilioni ya fedha katika ukalimani wa video zilizonakiliwa kwa Kiswahili kutafsiriwa kuwa Kiingereza. Pia watengenezaji wa filamu wametenga bajeti za kutafsiri video za Kiingereza kuwa Kiswahili.
Ili kufikia watazamaji na wasikilizaji wa kimataifa, runinga kama BBC na redio kama VOA zimekuwa zikiwalipa Wakenya kutafsiri Kiswahili cha Kenya kuwa Kiingereza na kuwainua kiuchumi Wakenya.
Ninawajua mamia ya wanachuo wa humu nchini ambao kila asubuhi huamkia kazi ya utafsiri kwenye vipakatalishi vyao na kulipwa kila siku na kampuni za Amerika na Uingereza. Kwao, hiyo ni ajira mwafaka ambapo hawahitaji kuwategemea wazazi wao kujikimu kimaisha.
Magazeti yetu ya Taifa Leo, Mwananchi na Mwanaspoti nayo yamewaajiri mamia ya wanahabari kuandika habari kwa Kiswahili, ili kuwafikia mamia ya wasomaji wa habari na makala, na kuwalipa mishahara inayowasaidia kujiendeleza kimaisha.
Yamkini kampuni za runinga na redio zote humu nchini zimewaajiri maripota, wahariri na maprodyusa wa Kiswahili. Hatua hii inatokana na kufahamu kuwa habari zinaposomwa kwa Kiswahili huwaingia watazamaji na wasikilizaji kwa mvuto wa aiba yake usiopatikana katika lugha nyingine.
Wasomi wa lugha na fasihi, wamejizolea fedha za maana kutokana huduma zao za utafiti wa Kiswahili katika vyuo vikuu nchini Tanzania, Kenya na Ujerumani.
Yaani kinavyoendelea kukua, kuna wasomi waliotwikwa jukumu la kufuatilia maendeleo hayo na kulipwa kwa kazi hiyo. Usiwasahau pia mamia ya waandishi wa vitabu vya Kiswahili nchini Tanzania na Kenya ambao wametia mfukoni mamilioni ya pesa kila mwisho mwaka kutokana na mauzo ya vitabu vyao vya riwaya, tamthilia, ushairi na kiada.
Kutokana na uandishi wao, Kiswahili kimeweza kufundishwa na wanafunzi kupewa baadhi ya vitabu kama kamusi au riwaya kujisomea, ili kuelewa misamiati mbalimbali ya lugha hii.
Wanapotua nchini, watalii kutoka mataifa ya kigeni hutumia baadhi ya muda wao kujifundisha lugha hii na kuwapa walimu wa Pwani ajira ya miezi mitatu hivi ili kukimanya Kiswahili kwa ajili ya mazungumzo ya kila siku na kufanya biashara na wauzaji wanaotumia Kiswahili wanapotemba Kenya au Tanzania.
Sina hakika umeziona lakini kunazo programu za simu zinazotoa huduma zake kwa Kiswahili na kueneza lugha hiyo mitandaoni. Labda itabidi usafiri Mombasa au miji ya Tanzania kujionea jinsi apu za huduma za kifedha, kiafya, uchukuzi na elimu zinawasaidia watumizi kuboresha maisha yao.
Kwa haya yote niliyotaja, hebu fikiria yakifanyika katika mataifa yote ya Afrika! Huo utakuwa mwisho wa mataifa ya Afrika kutegemea misaada kutoka mataifa ya kigeni kwani tutakuwa na lugha yetu rasmi ya mazungumzo ya kibiashara na kukifanya Kiswahili lugha ya kimataifa.
Check out Nicholas Rop Kiplangat’s-Profesa- profile on LinkedIn https://www.linkedin.com/in/nicholas-rop-kiplangat-5038051a0

Leave a comment